IDHAA YA KISWAHILI | DW
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo

Habari

Habari za Ulimwengu | 28.05.2020 | 15:00

Li atetea sheria mpya ya usalama kwa Hong Kong

Waziri Mkuu wa China Li Keqiang amesema leo sheria mpya kuhusu usalama wa taifa mjini Hong Kong inalenga kuimarisha uthabiti na ustawi wa muda mrefu wa mji huo. Akizungumza baada ya kumalizika kwa vikao vya bunge mjini Beijing, Li amesema sheria hiyo tata inayowalenga kuadhibu wale wanataka kujitenga, kudhoofisha nguvu ya dola na ugaidi inanuwia kuimarisha utekelezaji wa sera ya China moja. Wakosoaji wanasema uamuzi wa kulikwepa bunge la Hong Kong katika kupitisha sheria hiyo unaondoa misingi yote ya uhuru iliyoahidiwa na China wakati wa mkataba wa kuurejesha tena mji huo katika himaya yake mwaka 1997.

Hospitali za wagonjwa wa COVID-19 zimezidiwa nchini Indonesia

Jumuiya ya wafanyakazi wa afya nchini Indonesia imesema leo hospitali kwenye mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Surabaya zimezidiwa na wimbi jipya la visa vya virusi vya corona na zinalazimika kukataa kuwapokea wengine. Hospitali mbili za mji huo zilizotengwa kuwatibu wagonjwa wa COVID-19 zimefurika wagonjwa huku kukiwa na wasiwasi kuwa janga hilo linasambaa kwa kasi kutoka mji mkuu Jakarta kuelekea maeneo mengine ya Indonesia. Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyakazi wa afya katika jimbo uliko mji wa Surabaya amesema wanashuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa kuzidi idadi ya vitanda vilivyo hospitali. Tangu Mei Mosi idadi ya visa vya COVID-19 kwenye jimbo la Java Mashariki imepanda kwa asilimia 300 na kufikia wagonjwa 4,313 leo Alhamisi tofauti na ongezeko la asilimia 60 pekee katika mji mkuu Jakarta.

EU: Fedha za uokozi zitafungamanishwa na mageuzi

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imesema leo upatikanaji wa msaada wa kifedha kutoka fuko la uokozi wa uchumi kutokana na athari za virusi vya corona utafungamanishwa na mageuzi ya kiuchumi. Makamu wa Rais wa Halmashauri Kuu Valdis Dombrovskis amesema hatua hiyo itahakikisha fedha zitatumika vizuri na vipaumbele vilivyowekwa na Umoja huo vinaleta matokeo yaliyokusudiwa. Mpango huo wa uokozi uliopendekezwa na Umoja wa Ulaya unajumuisha Euro bilioni 500 za msaada na bilioni 250 nyingine za mikopo nafuu kunusuru kile kinachoweza kuwa mdodoro mbaya zaidi wa uchumi tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia. Ili kufapa fedha hizo, mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yatapaswa kuwasilisha mipango inayoanisha miradi ya kipaumbele na kisha kuidhinishwa na wanachama wote pamoja na Halmshauri kuu ya Umoja huo.

Kabuga kupelekwa mahakama ya kimbari Tanzania

Mmoja ya washukiwa wakuu wa ufadhili wa mauji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda Felicien Kabuga atasafirishwa kwenda katika mahakama maalum ya makosa ya uhalifu wa kivita mjini Arusha, Tanzania pindi taratibu zitakapokamilika. Uamuzi huo umetolewa leo na jaji mmoja wakati akijibu maombi ya kutaka Kabuga kuhamishwa kwa muda kwenda mjini The Hague kutokana na vikwazo vya kusafiri vilivyowekwa kukabiliana na viruis vya corona. Kabuga, moja ya watu waliosakwa kwa muda mrefu kutokana na dhima yake katika mauaji ya kimbari sasa anashikiliwa kwenye jela nchini Ufaransa tangu alipomatwa Mei 16 mjini Paris. Kabuga alipatikana na mashtaka ya kujibu mwaka 1997 katika mahakama ya maalum ya mauaji ya kimbari ya Umoja wa Mataifa kwa makosa 7 ikiwemo mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Ujerumani kuiwekea vikwazo Urusi kwa tuhuma za udukuzi

Wizara ya Mambo ya kigeni ya Ujerumani leo imemwita balozi wa Urusi kujadili uwezekano wa kuiwekea Moscow vikwazo kufuatia madai ya udukuzi ya mwaka 2015 dhidi ya bunge la Ujerumani, Bundestag. Taarifa ya wizara hiyo imesema balozi wa Urusi amearifiwa kuwaUjerumani inalenga kuuomba Umoja wa Ulaya kuiwekea vikwazo Urusi pamoja na raia wa nchi hiyo Dmitry Badin anayeshukiwa kuongoza udukuzi huo. Mapema mwezi huu Kansela Angela Merkel aliliambia bunge kuwa ana ushahidi wa Urusi kumlenga mara kadhaa kwenye mashambulizi ya udukuzi na kuongeza uwezekano wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Inaaminika kati ya mwaka 2012 na 2015 wadukuzi wa mtandaoni walifanikiwa kukusanya data za wabunge kadhaa wa Ujerumani pamoja na kupakua baruapepe mbili kutoka akaunti ya Kansela Merkel.

Iran yaionya Marekani kutokana na shughuli zake za kijeshi

Jeshi la walinzi wa mapinduzi ya Iran leo limeionya Marekani na uwepo wa jeshi lake la majini katika eneo la ghuba likiapa kuchukua hatua za kutanua operesheni zake kwenye maeneo yote ya kanda hiyo. Matamshi hayo yametolewa na mkuu wa jesh la majini la Iran Alireza Tangsiri wakati wa halfa ya kupokea zana mpya za kijeshi ikiwemo manuari na boti zinazokwenda kasi iliyofanyika kusini ya Iran. Jenerali huyo amesema kupitia vifaa vipya Jeshi la maji la Iran litafuatilia kwa karibu na kila wakati nyendo zote za wanajeshi wa Marekani kwenye eneo la Ghuba. Iran na Marekani zilikaribia mara mbili kutumbukia kwenye mzozo kamili wa kijeshi mwaka uliopita baada ya Washington kuituhumu Tehran kwa kuzitishia meli zake kwenye eneo la Ghuba

Wafanyakazi wa Nissan mjini Barceona waandamana

Mamia ya wafanyakazi leo wamechoma moto matairi na kuzingira tawi la kampuni kubwa ya kuunda magari ya Nissan mjini Barcelona baada ya kampuni hiyo kutangaza kuwa itakifunga kiwanda hicho mwezi Disemba. Kufungwa kwa tawi hilo na mengine duniani ni sehemu ya mpango wa mageuzi unaonuwia kupunguza gharama za uzalishaji kutokana na athari za virusi vya corona. Karibu wafanyakazi 1,000 waliofunikia nyuso mbali ya kuchoma moto maitiri pia waliifunga kabisia njia kuu ya kuingia na kutoka eneo la kiwanda. Uamuzi huo wa Nissan ni pigo kubwa kwa Uhispania inayoandamwa na ukosefu wa ajira na kuanguka kwa uchumi kutoka na mzozo wa virusi vya corona. Kampuni hiyo ya kuunda magari ya Japan, imetangaza kupunguza uzalishaji kwa asilimia 20 kufidia gharama za uendeshaji baada ya kurikodi hasara kwa zaidi ya miaka 11.

Matukio ya kisiasa

Matukio ya Afrika

Masuala ya jamii

Michezo

Habari kwa lugha ya Kiingereza

Matangazo
Tazama vidio 01:03